Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni katika Uendelezaji wa Kiswahili

Article

Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni katika Uendelezaji wa Kiswahili


Abstract

Makala hii ililenga kuchunguza mchango wa waandishi wa kazi za kubuni katika uendelezaji wa Kiswahili. Hili lilichochewa na ukweli kuwa waandishi ni miongoni mwa makundi muhimu katika ukuzaji wa lugha, mengine yakiwa: wanaisim, walimu, watafiti, wachapishaji, na wapenzi wa lugha. Hata hivyo, waandishi wa vitabu kuhusu maswala mbalimbali ya kinadharia, pamoja na uendelezaji wa lugha na fasihi yake ndio wametajwa zaidi. Mchango wa waandishi wa kazi za kubuni haujaangaziwa sana. Madhumuni mahsusi ya makala hii yalikuwa kuchanganua nafasi ambayo waandishi wa fasihi ya Kiswahili wameipa lugha hii katika kazi zao, pamoja na jinsi ambavyo nafasi hiyo inachangia katika ukuzaji wa lugha hiyo. Aidha, maelezo yametolewa kuhusu jinsi wamechangia kuwaathiri wasomaji wao kuhusu umuhimu wa Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya ushawishi wa kijamii inayoshikilia kuwa watu maarufu wana ushawishi mwingi unaowawezesha kuwaathiri wengine katika jamii. Waandishi wana sifa hizo na hivyo wanaweza kuathiri misimamo na mielekeo ya wasomaji wao kuhusu umuhimu wa lugha ya Kiswahili. Data ilikusanywa kwa kusoma kazi za kubuni za waandishi watatu wa fasihi ya Kiswahili walioteuliwa maksudi: Shaaban Robert, Wallah bin Wallah na Ken Walibora, pamoja na hojaji iliyotolewa kwa wanafunzi 40 na walimu 8 katika Chuo Kikuu cha Rongo. Vilevile, kazi za waandishi hao ziliteuliwa maksudi. Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kwamba waandishi hawa wameipa lugha ya Kiswahili nafasi ya kipekee kama sehemu ya maudhui katika kazi zao, na wamewachora wahusika wapenzi wa Kiswahili wanaokitetea Kiswahili, ambao wanawaathiri wahusika wenzao. Isitoshe, waandishi hawa wameathiri msimamo wa wanafunzi na walimu wa Kiswahili kuhusu Kiswahili kutokana na nafasi wanayokipa katika kazi zao. Makala inahitimisha kuwa, kwa mujibu wa nadharia ya ushawishi wa kijamii, waandishi ni kundi muhimu katika jamii lenye ushawishi mkubwa na wanapoendelea kuithamini lugha ya Kiswahili, watawaathiri wengine wengi kuwa na msimamo kama huo.

Get new issue alerts for Eastern African Literary and Cultural Studies